
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Leo Jumapili tarehe 7 Dey 1404 Hijria Shamsia (28 Desemba 2025), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandika moja ya mafanikio yake makubwa na muhimu zaidi katika anga za juu, ambapo kwa wakati mmoja setilaiti tatu za Iran zilizinduliwa angani kutoka kituo cha anga cha Vostochny nchini Urusi kwa kutumia roketi ya kubeba setilaiti ya Urusi aina ya Soyuz.
Kwa mujibu wa mipango iliyowekwa, setilaiti hizi zitawekwa katika kimo cha takribani kilomita 500 kutoka uso wa Dunia; mzunguko huu unafaa kwa ufuatiliaji wa mbali (remote sensing), upigaji picha za uso wa ardhi na ukusanyaji wa data za matumizi mbalimbali, na wakati huohuo unawezesha mawasiliano na uhamishaji wa data kwa haraka kati ya setilaiti na vituo vya ardhini.
Akizungumza leo jioni katika hafla ya uzinduzi wa setilaiti tatu za Iran mbele ya waandishi wa habari, Rais wa Shirika la Anga za Juu la Iran, Hassan Salarieh, alirejelea upanuzi wa mipango ya anga ya nchi hiyo na kusema kuwa Iran, kutokana na uwezo wake wa pamoja katika kubuni na kutengeneza setilaiti, roketi za uzinduzi pamoja na miundombinu ya kupokea na kuchakata data, imo miongoni mwa nchi 10 hadi 11 zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za juu.
Rais wa Shirika la Anga aliongeza kuwa kusainiwa kwa mikataba na makampuni na taasisi mbalimbali, pamoja na kufanikisha uzalishaji wa setilaiti zilizobuniwa na kutengenezwa ndani ya nchi, ni dalili ya maendeleo, upana na kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa sekta ya anga ya Iran.
Aidha, alisema kuwa kuingia kwa wadau wapya, hususan sekta binafsi na makampuni ya kiteknolojia (knowledge-based companies), ni ishara ya matumaini makubwa kwa mustakabali wa sekta ya anga ya nchi. Mwenendo huu, pamoja na kuendeleza teknolojia, pia unaweka msingi wa kuifanya sekta ya anga kuwa ya kiuchumi, jambo ambalo linazingatiwa kwa uzito mkubwa na serikali.

Kama inavyoonekana hapo juu ni Video ya tukio la uzinduzi wa setilaiti za Iran kwenda anga za juu kutoka kituo cha anga cha Vostochny
Rais wa Shirika la Anga za Juu la Iran, akieleza kuwa bidhaa na ripoti zinazotokana na picha za setilaiti zinaweza kuleta thamani kubwa ya ziada, alisisitiza kuwa kwa mitazamo mbalimbali inawezekana kufafanua thamani ya kiuchumi kwa sekta ya anga ya nchi, jambo ambalo lina mchango muhimu katika uendelevu na ukuaji wa sekta hiyo.
Salarieh, akirejelea nafasi ya Iran katika sekta ya anga ya dunia, alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imo miongoni mwa nchi 10 hadi 11 bora duniani ambazo kwa wakati mmoja zinamiliki uwezo wa kubuni na kutengeneza setilaiti, vyombo vya kuzindulia setilaiti (launch vehicles), pamoja na miundombinu ya uzinduzi, upokeaji wa data na uchakataji wa picha, na kwamba kwa miaka mingi imekuwa ikifanya kazi kwa mwendelezo katika uwanja huu.
Aliendelea kusema: jambo lililo muhimu kwetu ni kuongeza idadi ya setilaiti, kuinua usahihi na ubora wake, na kuendeleza aina mbalimbali za setilaiti zikiwemo za mawasiliano, ufuatiliaji (sensing), rada na upigaji picha. Sekta ya anga duniani ni ya ushindani mkubwa, na nchi zilizoingia katika uwanja huu zinaendelea kuongeza matumizi yao ya anga.
Rais wa Shirika la Anga za Juu la Iran, akisisitiza umuhimu wa kudumisha kasi ya maendeleo, alisema kuwa nchi mpya zimeingia katika ushindani wa anga, na nchi nyingi ambazo hapo awali hazikuwa na nafasi katika sekta hii sasa zimeanza kuwekeza. Hivyo, Iran nayo inapaswa kuendelea na mkondo wa maendeleo kwa kutegemea teknolojia za ndani, rasilimali watu wa kitaifa na kwa kasi ya juu.
Kuhusu nafasi halisi ya Iran miongoni mwa nchi za anga, Salarieh alisema kuwa kubainisha cheo kamili kati ya nchi 10 au 11 si jambo rahisi; hata hivyo, alibainisha kuwa kati ya takribani nchi 200 duniani, chini ya asilimia tano pekee ndizo zenye uwezo kamili wa anga, na Iran ni miongoni mwa nchi hizo.
Mwisho, akirejelea sifa za kiufundi za setilaiti zilizozinduliwa, alisema kuwa setilaiti zilizozinduliwa hivi karibuni na zile za awali zinahesabiwa kuwa miongoni mwa setilaiti za kisasa kwa upande wa usahihi na ubora, na katika nyanja ya upigaji picha zimefikia kiwango cha usahihi wa takribani mita 15, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la uwezo wa kiufundi wa nchi.
Your Comment